Wakazi wa mtaa wa Ngobedi Kata ya Zingiziwa wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam wamewagomea makarani wa sensa kuwahesabu kutokana na kuwepo kwa mgogoro wa mipaka katika eneo hilo.
Wakizungumza Agosti 23 viongozi wa maeneo hayo waliofika ofisi ya Serikali ya Mtaa kutoa malalamiko yao, wamesema mgogoro huo umekuwepo tangu mwaka 2018 na haujawahi kupatiwa ufumbuzi.
Eneo hilo linapakana na Wilaya ya Kisarawe upande wa Magharibi na Wilaya ya Mkuranga upande wa Kusini zote za mkoani Pwani, limezua mgomo huo kutokana na utata wa mipaka.
Mjumbe wa Shina namba 23, Daniel Masanja amesema hata kipindi cha uandikishaji anuani za makazi watu walipigwa, kujeruhiwa na kufunguliwa kesi mbalimbali kutokana na kugoma kuandikishwa kama wapo upande wa Kisarawe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Miundombinu, Issa Kambona ameonesha aibu yake baada ya kutokea kwa tukio hilo la kususia sensa katika Kata ambayo anaishi Makamu wa Rais, Philip Mpango, na kwa maoni yake kata hiyo ingetakiwa iwe ya mfano katika shughuli hiyo.
Naye Salma Sultan amesema huduma zote za kijamii wanazipata Kata ya Zingiziwa ambayo ipo Mkuranga na kushangaa wanahesabiwa katika Kata ya Mazimbu ambayo ipo Kisarawe.
“Tunavyojua sensa ni moja ya sababu ni kujulikana kuna watu wangapi ili hata baadaye huduma zitakapotolewa ijulikane wanahudumiwa wangapi, sasa kwa utaratibu huu inamaana tutaachwa pembeni na bajeti yetu haitakuwepo huko serikalini,” amesema Salma.
Kwa upande wake Mwenyekiti Serikali ya Mtaa ya Zingiziwa, amesema waliomba viongozi wa juu kuushughulikia mgogoro huo kwa muda mrefu, lakini hawajafanya hivyo na hata wakifika kweye eneo husika wanajikuta wakigombana wenyewe kwa wenyewe.
Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Nickson Simon ameomba muda kufuatilia suala hilo.
Chanzo:Mwananchi