Hatua ya Wizara ya Habari, kuitisha kikao na Wanahabari na kisha kupitia mchakato wa mapendekezo ya sheria za habari, ni moja kati ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Hayo yamebainishwa na Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena wakati akizungumza na Kituo kimoja cha Habari jijini Dodoma mapema mwezi huu wa Agosti, 2022.

Amesema, kitendo cha mapendekezo ya wadau wa habari kupita, ni mjadala mpana lakini kitendo cha Wizara kukutana na wadau wa habari na kupitia vifungu,inaonesha nia ya Serikali katika kuwasikiliza Waandishi wa Habari na kufanyia kazi mapendekezo yao.

“Sisi kama wadau wa habari tunaamini tunakwenda kufanikiwa kwa kuwa, hata Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ana hisia chanya katika mchakato huo ambao umewagusa wanatasnia wengi,’’ amesema Meena.

Aidha, Meena ameongeza kuwa miongoni mwa mapendekezo ya wadau wa Habari katika mabadiliko ya sheria za habari nchini, ni pamoja na kuuheshimu uamuzi wa Mahakama katika mashauri yake yanayotolewa hukumu.

Amesema, “Hii inatokana na kwamba licha ya baadhi ya vyombo vya Habari kushinda kesi Mahakamani lakini wakimaliza vifungo vyao, Idara ya Habari Malelezo bado iligoma kuwapa leseni ili kuendelea na kazi zao za kila siku za Kihabari.”

Meena ameongeza kuwa, “Kuna gazeti (MwanaHalisi) licha ya kushinda kesi mahakamani, hawakupewa leseni ya kuendelea na uchapaji habari na ikumbukwe ni hao hao pia hata walipomaza kifungo bado hawakupewa leseni, jambo hili sio sawa hata kidogo.”

Hata hivyo, Meena amefafanua kuwa Wadau wa Habari nchini wamependekeza kwamba, Mahakama inapotoa hukumu juu ya jambo fulani, basi Serikali inapaswa kutekeleza jambo hilo tofauti na ilivyo sasa ambapo hukaa kimya bila kuchukua hatua zozote.

“Mkurugenzi wa Habari Maelezo anatumia sheria ile ile ambayo sasa inalalamikiwa ya kuwa na uamuzi wa kutoa leseni kwa chombo cha habari ama kutotoa kwa utashi wake, katika hili tunapendekeza gazeti likishasajiliwa basi liendelee na kazi kwa kufuata taratibu zilizopo,” amesisitiza Meena.

Majirani wa Makamu wa Rais wagomea Sensa
Kaseja: Sina mpango wa kustaafu soka