Mamlaka ya Serikali nchini Togo, imetangaza kuachiliwa kwa wanajeshi watatu wa kike wa Ivory Coast waliokuwa wamezuiliwa nchini Mali, tangu mwezi Julai 2022.
Wanajeshi hao watatu, waliachiliwa kwa misingi ya kibinadamu wakiwa ni sehemu ya kundi la wanajeshi 49 wa Ivory Coast waliozuiliwa mjini Bamako tangu Julai 10, 2022.
Togo, imekuwa ikipatanisha mgogoro kati ya Mali na Ivory Coast, huku majadiliano ya sasa yakilenga kuachiliwa kwa wanajeshi 46 waliosalia.
Kwa mujibu wa mamlaka ya Mali, wanajeshi hao wa Ivory Coast wanatuhumiwa kuwa mamluki huku mamlaka ya Ivory Coast ikidai walikuwa kwenye misheni ya kusaidia vikosi vya Umoja wa Mataifa, nchini Mali.
Mamlaka ya Ivory Coas, imeahidi kufuata sheria za Mali na Umoja wa Mataifa kuhusiana na kutumwa kwa vikosi vya kijeshi nchini humo.
Mali, pia imeishutumu Abidjan kwa kuchochea nchi za Afrika Magharibi kuimarisha vikwazo dhidi ya wanajeshi wa Mali kufuatia mapinduzi mawili tangu 2020.