Mwanamume mmoja, aliyetambulika kwa jina la Mahesh Tiwari (47), amewaua watu watano wa familia yake, wakiwemo binti zake wadogo watatu na mama yake mzazi, kufuatia kuzuka kwa mabishano na mkewe juu ya uandaaji wa kifungua kinywa.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi wa Dehradun (SSP), Dilip Singh Kunwar amesema tukio hilo limetokea Agosti 13, 2022 katika eneo la Ranipokhri ambapo mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na kisu cha jikoni kilichotumika katika mauaji hayo.

Amesema, marehemu wote wametambuliwa akiwemo mama wa mtuhumiwa Bi. Beetan Devi (75), mkewe Bi. Neetu Devi (36), na binti zake watatu ambao ni Aparna Tiwari (13), Swarna Tiwari (11), ambaye ana ulemavu tofauti na Annapurna Tiwari (9).

Mtuhumiwa Mahesh Tiwari, anayedaiwa kuwaauwa watoto wake watatu, mama yake mzazi na mkewe. Picha na Theghanaweb.com

“Bwana Tiwari hana kazi na kaka yake mkubwa Umesh anayefanya kazi Uhispania hutuma pesa kila mwezi kwa matumizi ya familia yake inayoishi katika eneo la Nagagher anapoishi mtuhumiwa na alihamia hapo mwaka 2012, baada ya kifo cha baba yake Dinesh Kumar,” amesema SSP Kunwar.

Ameongeza kuwa, “Mahesh ni mtu wa kidini sana na alikuwa akihusika katika huduma za kidini mara nyingi na jambo lililotokea linahusishwa na mvutano kati yake na mkewe, ambaye alitaka Mahesh apate kazi na kuleta pesa nyumbani.”

Inadaiwa kuwa, Siku ya tukio majira ya saa moja asubuhi, mtuhumiwa alikuwa akijiandaa kuwapeleka binti zake shuleni na ndipo kukatokea kupishana kwa kauli kati yake na mkewe ambaye alimtaka awahi kurudi ili kumsaidia kuandaa kifungua kinywa.

Polisi katika eneo la tukio. Picha na theghanaweb.com

Kamanda huyo wa Polisi, aliongeza kuwa mabishano mengine ni juu ya kutengeneza silinda ya gesi na Tiwari alipojaribu kuibadilisha kulizuka ugomvi mkubwa na mkewe ndipo mtuhumiwa Tiwari alichukua kisu cha jikoni kumkata mke wake koo.

Amesema, “Baadaye, Tiwari aliwauwa binti zake watatu kisha kumuua mamake mzazi ambaye aliripotiwa kuwa na matatizo ya kisaikolojia na akajifungia ndani na ndipo majirani walisogea na kuona damu nyingi eneo la tukio na kuita Polisi.”

Mtuhumiwa Mahesh Tiwari, amekiri kuhusika na mauaji hayo, ambapo Polisi imesema inakamilisha taratibu ili iweze kumfikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili, ambapo pia imewataka Wananchi kuzuia hasira zao kwani zinaweza kuharibu mifumo ya maisha.

Majaliwa:Barabara mzunguko Dodoma iishe
Wanajeshi waliokuwa kizuizini waachiliwa huru