Wakenya walisubiri kwa hamu uamuzi wa Mahakama ya Juu wa hii leo Jumatatu Septemba 5, 2022 kuhusu kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais, baada ya kupitia siku kadhaa za sintofahamu ya kisiasa nchini humo.
Naibu Rais, William Ruto alitangazwa mshindi wa kinyang’anyiro hicho kilichopiganiwa vikali, na kupata ushindi kwa tofauti ndogo ya chini ya asilimia mbili ya pointi dhidi ya Raila Odinga, ambaye ni mwanasiasa mkongwe wa upinzani anayeungwa mkono na chama tawala.
Odinga, aliwasilisha ombi katika mahakama ya juu ya Kenya mwezi uliopita, akidai kulikuwa na udanganyifu katika mchakato wa kujumlisha kura na kudai kwamba alikuwa na “ushahidi wa kutosha” kuonyesha ukweli kuwa alishinda uchaguzi wa Agosti 9, 2022.
Vyombo vya Habarai nchini Kenya vimepambwa na vvichwa vya habari tofauti kama “Siku ya Hukumu,” kilicho ukurasa wa mbele wa Gazeti la The Standard, huku Gazeti la People Daily likiandika “Moment of Truth”.
Ingawa siku ya kupiga kura ilipita kwa amani, matokeo hayo yalizua maandamano ya hasira katika baadhi ya ngome za Odinga na kuna hofu kwamba mzozo wa muda unaweza kuzidisha hali mbaya ya kiuchumi na kusababisha ghasia katika nchi yenye historia ya machafuko baada ya uchaguzi.
Mahakama itachunguza iwapo dosari zozote zilitosha kubatilisha uchaguzi, kama ilivyokuwa katika kura ya urais ya Agosti 2017, ambayo Odinga pia alipinga, na inatarajia kutoa maamuzi hii leo hapo baadaye.