Serikali nchini, imemuelekeza Katibu wa Wizara ya Ardhi kuchukua hatua kwa Makamishna wasaidizi wa ardhi na wasaidizi wao ambao waneshindwa kukidhi matarajio kwa kufanya kazi kwa mazoea.

Agizo hilo, limetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula hii leo Septemba 6,2022 Jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao kazi cha Makamishna wasaidizi wa ardhi wa mikoa.

Amesema, watumishi hao wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea, ikiwemo hali ya kuogopana, kulilindana na hivyo kuathiri utendaji wa kazi na kuleta sintofahamu kwa wananchi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula

Amesema pamoja na hatua za kinidhamu zilizochukuliwa kwa baadhi ya watumishi saba walioachisha kazi bado hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa kwa wengine ili kuleta usawa na uwajibikaji unaozingatia maadili ya umma.

Kuhusu mashauri ya kinidhamu, ambayo yanaendelea Waziri Mabula amesema, “Naelekeza yakamilishwe haraka na Mikoa ambayo tunakamilisha taratibu za kinidhamu kwa watumishi wa Mbeya, Dar es Saaam, Mwanza na Arusha na Lindi.”

Hata hivyo, amedai kubaini uwepo wa watumishi wanaojihusisha na vitendo vya udanganyifu kwenye zoezi la uthamini wa mali, ambapo majina yao yanafanyiwa kazi ili kuwachukulia hatua za kinidhamu.

Habari kuu kwenye magazeti ya leo Septemba 07, 2022
Ajali ya basi: 45 wanusurika kifo