Bunge la Togo, limerefusha kwa miezi sita hali ya hatari katika eneo la Savannah lililopo kaskazini mwa nchi hiyo linalipakana na nchi ya Burkinafaso, ambalo limekuwa likikumbwa na uvamizi wa makundi ya wanajihadi.
Huku makundi hayo ya Jihadi, yanayoendesha shughuli zake katika Sahel yakionekana kuelekea katika pwani ya Afrika Magharibi hatua kwa hatua, kaskazini mwa Togo imekumbwa na mashambulizi matano tangu Novemba 2021.
Hali ya hatari, imeongezwa kutoka ilipotangazwa Juni, 2022 na rais wa Togo hadi Machi 2023 katika mkutano wa Bunge mjini Kara, takriban kilomita 400 kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo Lome.
Katiba ya nchi hiyo, inahitaji idhini ya bunge ili kuongeza muda wa hali ya hatari huku Spika wa Bunge Yawa Djigbodi Tsegan akisema, “Lengo letu ni kuvipa vikosi vya ulinzi na usalama njia zinazofaa kukomesha tishio hilo.”
Kwa mujibu wa Waziri wa Usalama wa Togo, Damehame Yark, amesema hali ya hatari inaunda masharti ya hatua za kiutawala na uendeshaji na kusena upo umuhimu wa uendeshaji mzuri wa operesheni za kijeshi na kurejesha amani katika eneo hilo.
Shambulio baya zaidi nchini Togo, lilifanyika mwezi Julai ambapo watu wenye silaha walishambulia vijiji vinne, na jeshi kuripoti uwepo wa vifo na majeruhi bila kutoa idadi kamili ingawa vyombo vya Habari vikiripoti kuwa watu 15 hadi 20 waliuawa.