Jeshi la Polisi linawashikilia Wauguzi watatu, wa kituo cha afya wanaotuhumiwa kuhusika na upotevu wa viungo vya mtoto mchanga aliyefariki muda mfupi baada ya kufikishwa na wazazi wake kwa matibabu Hospitalini.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo la nchini Nigeria, iliyotolewa kwa vyombo vya Habari mapema wiki hii imeeleza kuwa, mtoto huyo alifikishwa katika hospitali ya Asaba, iliyopo mji mkuu wa Jimbo la Delta Oktoba 9, 2022.
Imesema, mara baada ya Wazazi wa mtoto huyo kumfikisha mtoto huyo Hospitalini majira ya jioni, Daktari wa watoto alimumfanyia vipimo na kuthibitisha kuwa tayari alikuwa amefariki.
Siku iliyofuata (Jumatatu Oktoba 10, 2022), inasemekana familia ilimchukua mtoto huyo kwa ajili ya taratibu za mazishi na badaye waligundua mapungufu katika mwili wa mtoto kwamba alitolewa macho, pua na sikio.
“Inasemekana wazazi walibeba mwili wa mtoto ila siku ya Jumatatu asubuhi, wazazi walirudi wakiishutumu hospitali kuondoa macho, pua na masikio na walikuja na Polisi waliokamata baadhi ya wauguzi,” alisema shuhuda wa tukio hilo.
Afisa Uhusiano wa Umma wa Polisi wa jimbo hilo, DSP Bright Edafe, alithibitisha kukamatwa kwa wafanyikazi hao amesema “Ni tukio la kweli ila sijapata undani wake, lakini tulipata taarifa kuwa mtoto huyo alipewa rufaa ya kwenda hospitali hapo baada ya ile ya awali kuzidiwa uwezo wa kitabibu wa tatizo alilonalo, maiti imehifadhiwa na uchunguzi unaendelea.”