Aliyewahi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Harison Mwakyembe hii leo Oktoba 12, 2022 ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati ya watu saba itakayofuatilia chanzo cha kufeli kwa wanafunzi wengi wa mitihani ya mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST).

Uteuzi wa Dkt. Mwakyembe umefanywa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro jijini Dodoma ambapo sasa ataungana na Wajumbe wa kamati hiyo akiwemo aliyewahi kuwa mshauri wa Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, Jaji Mstaafu, Cililius Matupa na Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma wa Zanzibar, Rashid Asaa.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro akiongea mbele ya Waandishi wa Habari.

Wengine walioteuliwa ni pamoja na Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Gloria Kalabamu, Wakili mwandamizi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Alice Mtulo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Dar Stock Exchange, Mary Mniwasa na Mwanafunzi aliyehitimu LST, John Kaombwe na wanatarajia kufanya kazi hiyo kwa siku 30.

Kamati hiyo, imeundwa kufuatia mjadala ulioibuka kufuatia taarifa za kiwango cha idadi kubwa ya wanafunzi waliofeli mtihani wa mwisho kwa elimu ya vitendo katika taasisi hiyo ambapo sasa Kamati itakabidhiwa hadidu rejea na Katibu Mkuu wa Wizara Katiba na Sheria, Mary Makondo Oktoba 13, 2022.

DAR24 Team 'yanoa makali' Ufukweni
Rais Samia kuongoza mjadala wa kitaifa Nishati Safi ya Kupikia