Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limewataka wazalishaji wa Pombe Kali na Mvinyo Wilayani Karagwe, kuzalisha bidhaa zao kwa ubora, ikiwemo kufuata sheria zinazomlinda mtumiaji ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza na kujihakikishia soko la ndani na nje.

Akiongea katika semina, iliyoandaliwa na shirika hilo kwa wazalishaji wa bidhaa hizo, Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Mhandisi Joseph Mwaipaja amesema uzingatiaji wa ubora na usalama wa mtumiaji utasaidia kuwa na bidhaa bora na kulifikia Soko la Kimataifa.

Amesema, bidhaa nyingi zimekuwa zikizalishwa nje ya ubora husababisha kutokufanya vizuri katika solo la Kimataifa hali inayofanya kutokuongeza kipato kwa wazalishaji na kuongeza kuwa bidhaa nyingi zisizo na ubora zimekuwa zikileta Madhara kwa watumiaji na kupunguza nguvukazi kwa jamii.

Awali, Mgeni Rasmi katika mafunzo hayo Mkuu wa wilaya ya Karagwe, Mwl. Juliet Binyura aliwataka wenye viwanda kutokujihusisha na uzalishaji wa Pombe ya Moshi (Gongo), ambayo imekuwa ikileta madhara kwa watumiaji.

Binyura amesema, Serikali itaendelea kusisitiza na kusimamia uzalishaji wa bidhaa zenye ubora na kusimamia masoko kwani Wilaya ya Karagwe ina viwanda vingi vinavyozalisha Pombe Kali na Mvinyo, ambavyo vimekuwa vikitoa ajira kwa wananchi.

Wakiongea kwa nyakati tofauti, baadhi ya wazalishaji wa vinywaji hivyo wamesema mafunzo hayo yamekuwa mwanga na njia ya kuweza kuyafikia malengo yao na kwamba kwa siku za nyuma walizalisha bidhaa zao kienyeji na bila kufuata sheria na kufitia mafunzo hayo watafanya mapinduzi ya uzalishaji ulio Bora zaidi.

Rais Samia kuongoza mjadala wa kitaifa Nishati Safi ya Kupikia
Ahmed Ally: Njooni Kwa Mkapa tuweke rekodi mpya