Klabu ya Simba SC imejiandaa kuweka Rekodi mpya Uwanja wa Benjamin Mkapa itakapocheza mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Primero de Agosto ya Angola.

Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo, baada ya kushinda ugenini mwishoni mwa juma lililopita (Jumapili-Okatoba 09), huku ikitarajia kuendeleza ilipoishia na kutinga Hatua ya Makundi Jumapili (Oktoba 16).

Maneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amesema wamejipanga kutoa hamasa kwa Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo ili kwenda kuandika Rekodi Mpya Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumapili (Oktoba 16).

Amesema lengo kuu ya Simba SC ni kuhakikisha Mashabiki na Wanachama wanaujaza Uwanja huo mkubwa nchini Tanzania, huku wakichagizwa na aina mbalimbali za kuishangilia timu yao yenye uchu wa kurejea Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, baada ya kushindwa kufanya hivyo msimu uliopita.

“Upande wa hamasa tunaendelea kupita kwenye vyombo vya habari na kupita mitaani, siku ya ijumaa tutakuwa Temeke, tutazunguka na kispika twende tukaiunge mkono timu yetu. Tukio la kipekee tutakuwa na chakula cha pamoja, biryan la kwenda hatua ya makundi.”

“Siku ya mchezo milango itafunguliwa mapema, kutakuwa na burudani kabla ya mchezo. Tutagawa bendera uwanja mzima kwa kila shabiki wa Simba jukumu lake ni kupeperusha. Lengo letu ni kutengeneza hali ya kuvutia uwanjani ili ionekane ni mechi ya Simba.”

“Kila shabiki wa Simba afanye kila anachoweza yeye binafsi kuja uwanjani na muhimu zaidi kuhamasisha wenzake kuja uwanjani. Lengo letu ni kuingia makundi tukiwa watu wasiopungua 60,000.”

“Kwa wale ambao wana maflashflash ya kuwakawaka wanaruhusiwa kuja nayo. Muhimu liwe jekundu ili kuendana na rangi yetu.”

“Tiketi zinaendelea kununuliwa lakini bado kasi ni ndogo, tunajua asili yetu Watanzania ni kununua siku za mwisho, tunategemea manunuzi yatakuwa makubwa kuanzia kesho. Siku ya mchezo tutauza pia tiketi uwanjani. Tunasisitiza watu kununua mapema.”

“Kwa anayetaka kununua Platinum muda ni sasa mpaka naingia hapa zilikuwa zimebaki kama 20 hivyo inabidi kuwahi mapema kabla hazijaisha.”

“Tutaingia kwenye mchezo tukijua haujaisha, bado tunajua tunatakiwa kupambana kwa dakika zingine 90. Mechi haijaisha.”

“Kocha Mgunda anafanya vizuri na kila mmoja anaona. Simba tuliyokuwa tunaitaka tunaiona kwake. Namna watu wanashambulia, wanavyokaba na mpira unavyotembea. Bodi ya Wakurugenzi itafanya maamuzi lakini ametupa tunachotaka na tunaamini atatupeleka makundi.” amesema Ahmed Ally

Wazalishaji Pombe kali 'waumwa sikio' Karagwe
Rais Samia atarajia kufanya ziara Kigoma