Wanasheria na baadhi ya wadau wametaka utafiti ufanyike kubaini chanzo cha anguko kwenye mtihani wa uwakili katika Shule Kuu ya Sheria Tanzania (LST).

Pendekezo hilo na mengine yamekuja kufuatia matokeo mabaya katika mtihani uliofanywa mwaka huu (2022), na wanafunzi 633 ambapo katika mtihani huo wanafunzi 26 sawa na asilimia 4.1, pekee ndio waliofaulu.

Aidha, Wanafunzi 342 wametakiwa kurudia baadhi ya masomo, na wengine 265 sawa na asilimia 41.9, wakifeli na kukatishiwa masomo ambapo katika mwaka wa masomo 2018/2019 kati ya wanafunzi 1,735 waliofanya mtihani 347 walifaulu kuendelea, 484 walirudia mitihani na 468 kufeli.

Lango la kuingilia Shule ya Sheria.

Katika mwaka wa masomo 2016/17-2017/18 kati ya wanafunzi 2,662 waliofanya mtihani 445 (sawa na asilimia 16.72) walifaulu, 1,611 (sawa na asilimia 60.53) walirudia na 606 (sawa na asilimia 22.76) walifeli ambapo uongozi wa shule hiyo umejibu malalamiko ya wadau ukifafanua changamoto zilizopo, ikiwemo ya maandalizi duni waliyoyapata wanafunzi hao katika vikuu vikuu mbalimbali walivyosomea shahada zao.

Jaji wa Mahakama Kuu, Gabriel Malata alisema jawabu la changamoto zote zinazoikabili hatua hiyo ya taaluma ya sheria litapatikana iwapo utafanyika utafiti na kusema, “Kabla hatujaenda mbali lazima tujue tatizo na kuliwekea nguvu, bila shaka ufumbuzi utapatikana. Tujue kwanini hali hii inajitokeza? Mtalaa unaweza kuwa sehemu ya tatizo lakini tukifanya utafiti tutabaini na mengine mengi,” alisema.

Kwa kuwa jambo hilo linahusu maisha ya watu, Jaji Malata alisema si vema mwanafunzi anahitimu shahada kisha anakwama miaka kadhaa katika Shule Kuu ya Sheria, sababu anafeli.

Mbeya City imeingia kimataifa 
PSSSF yatumia Bilioni 200 pensheni kwa mwezi