Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Queen Sendiga amewataka Wakuu wa Wilaya, kuhakikisha mikataba waliyosaini ya utekelezaji afua za lishe inatekelezwa hadi ngazi ya watendaji kabla ya Oktoba 25, 2022 ili kupunguza kiwango cha udumavu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano, ambapo kwa Mkoa wa Rukwa kipo kwa asilimia 47.9.

Sendiga, ameyasema hayo mjini Sumbawanga hii leo Oktoba 19, 2022 wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya utekelezaji afua za lishe kati yake na Wakuu wa Wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo.

Amesema, “Maelekezo yangu kwa Wakuu wa Wilaya, mkasimamie wilaya zenu kuhakikisha fedha zilizopangwa kutekeleza afua za lishe zinatolewa kwa wakati. Aidha, taasisi zote zinazoshughulikia suala la lishe katika mkoa zijulikane ili iwe rahisi kufuatilia mipango yao utekelezaji.”

Awali, kizungumza kwa niaba ya Madiwani wa mkoa wa Rukwa, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga, Justin Malisawa alisema Halmashauri za mkoa huo zitaendelea kutenga na kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji afua za lishe ili kukabiliana na tatizo la udumavu na utapiamlo unaothiri afya ya watoto chini ya miaka mitano.

Malisawa aliongeza kuwa, “Sisi madiwani tutaendelea kuhakikisha kila matumizi ya halmashauri ya miezi mitatu fedha za lishe zinatengwa na kupelekwa katika utekelezaji wa agenda za lishe .Suala la lishe endelevu litaendelea kupewa kipaumbele.”

Kupitia tathmini, iliyofanywa jijini Dodoma Septemba 30, 2022 Mkoa wa Rukwa ulitangazwa kushika nafasi ya kwanza kitaifa kwa utekelezaji mzuri wa afua za lishe, huku Mratibu wa Mradi wa Lishe Endelevu Mkoa wa Rukwa, Maria Machilu akisema vikao vya kamati za lishe vipewe kipaumbele ili kuwezesha jamii kushiriki upangaji wa mikakati ya kupunguza udumavu, ikiwemo elimu ya lishe bora.

Hakuna wa kunipiga marufuku: Mtoto wa rais ajibu
Serikali yaendeleza juhudi kuimarisha utawala bora