Kiungo Mkabaki kutoka DR Congo na Klabu ya Mtibwa Sugar Pascal Kitenge Kadyamba amesema hana kinyongo na Mwamuzi Tatu Malongo aliyemuonyesha Kadi Nyekundu wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba SC, uliopigwa jana Jumapili (Oktoba 30) Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Simba SC iliyokua mwenyeji wa mchezo huo, iliibuka na ushindi wa mabao 5-0, na kujiongezea alama katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kitenge ambaye aliadhibiwa kwa Kadi Nyekundu kufuatia kosa la kumkanyaga kwa makusudi Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC Pape Ousman Sakho, amesema kilichotokea ni sehemu ya mchezo, hivyo amepokea alichokutana nacho Uwanjani.

Amesema kadi nyekundu ni sehemu ya mchezo, lakini hakudhamiria kufanya alichokifanya kwa Pape Sakho, japo aliumizwa na kilichomfika kwa sababu anajua aliigharimu timu yake na kufikia hatua ya kupoteza mchezo.

“Kadi nyekundu ni sehemu ya mchezo, haijanikatisha tamaa kabisa japo sikukusudia kufanya vile, ilitokea bahati mbaya na ninakiri kujutia tukio lile,”

“Ninajua adhabu yangu imeigharimu timu kwa kiasi kikubwa hadi kupoteza mchezo kwa idadi kubwa ya mabao, tumekubaliana na matokeo, lakini ninaamini Kocha wetu atatumia mbinu mpya katika maandalizi yetu kabla ya kucheza dhidi ya Azam FC.” amesema Kitenge.

Mtibwa Sugar watakua wenyeji wa Azam FC katika Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro, mwishoni mwa juma hili.

Deo Kanda: Simba SC imetumia uzoefu
Shambulizi la ghafla laua wanajeshi 13