Mbunge wa Nzega Vijijini (CCM), Hamisi Kigwangala amemtaka Waziri wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda kujitafakari ili kumpa nafasi Rais afanye uteuzi wa mtu mwingine takayemsaidia katika nafasi hiyo kutokana na kulidanganya Bunge, Watanzania na vijana wanaosubiri mikopo.
Kigwangala ametoa kauli hiyo hii leo Novemba 7, 2022 wakati akichangia mjadala wa taarifa ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii ambayo iliwahoji bodi ya Mikopo kwa elimu ya Juu (HESLB), kufuatia agizo la Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson juu ya kauli ya Waziri Mkenda kwamba Bodi hiyo inamuangusha.
Amesema anamuomba Waziri Mkenda kuomba radhi mbele ya Bunge na Watanzania, na pia ajitathimini kama anatosha kwenye nafasi hiyo ili kumsaidia Rais, ambapo Spika wa Bunge alimtaka Kigwangala kujikita katika taarifa ya Kamati.
Spika Tulia amebainisha kuwa, baadhi ya mambo aliyoyasema Kigwangala hayamo kwenye taarifa ya Kamati ikiwemo la Waziri kusema uongo hivyo akamuomba ajikite kwenye taarifa.
Mapema hivi karibu, kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii Mbunge Hamis Kigwangala alimtuhumu aliyekuwa Katibu Mkuu wake katika Wizara ya Maliasili na Utalii kwamba hana mahusiano mema na watumishi katika Wizara yake.
Itakumbukwa kuwa, Mkenda na Kigwangala waliwahi kuhudumu Wizara moja ya Maliasili na Utalii na kuingia katika mgogoro baada ya kutokuelewana na hivyo kupelekea Rais, (Hayati), John Joseph Pombe Magufuli kuingilia suala hilo.