Jeshi la Polisi, Kikosi cha kuzuia na kupambana na wizi wa mifugo, migogoro ya wakulima na wafugaji nchini kwa kushirikiana na hifadhi ya Taifa Tarangire limekamata Ng’ombe 2035 walioingia hifadhini kinyume cha Sheria.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kikosi cha kuzuia wizi wa mifugo nchini kamishina msaidizi wa Polisi ACP. Simon Pasua amesema kutokana na tukio hilo Jeshi linawashikilia watuhumiwa sita kwa kosa la kuingiza na kulisha mifugo hiyo ndani ya hifadhi.
Amesema, Watuhumiwa waliokamatwa ni Muliyo Lekashu (25), Moringe Mpeleke (30),Sabaya Sumuni (38), Lemburis Roika (45),Terengo Kondeki (70),Saruni Rosio (43) wote ni wakazi wa Emboreti wilaya ya Simanjiro.
Aidha, Kamanda Pasua amebainisha kuwa Jeshi hilo linaendelea na upelelezi na mara baada upelelezi kukamilika watuhumiwa watafikishwa katika vyombo vya sheria na kutoa wito kwa wafugaji kufuata sheria za matumizi bora ya ardhi.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa Tarangire, William Maregesi amesema wao kama wadau wakubwa wa uhifadhi watawachukulia hatua wale wote watakao husika na uharibifu wa rasilimali za Taifa.