Abiria 57 waliokuwa wakisafiri na basi la kampuni ya Al-Saedy, wamenusurila kifo katika ajali iliyotokea eneo la Kitungwa Mkoani Morogoro, baada ya basi hilo lililokua likitokea Kilosa kuelekea Mkoani Dar es Salaam kupinduka.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilim amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa Dereva wa basi la Ally’s Star, lililokua likitokea Dar es Salaam kuelekea Mwanza, kutaka kuyapita magari yaliyopo mbele yake bila kuchukua tahadhari.
Amesema, kufuatia hali hiyo, Dereva wa basi la Al Saedy alimkwepa na ndipo likapinduka na Dereva aliyesababisha ajali hiyo anashikiliwa na Polisi huku Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Emanuel Ochieng akisema abiria 17 wamepata majeraha madogo isipokuwa Kondakta wa basi hilo ambaye amekimbizwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa matibabu zaidi.
Ajali hiyo, imetokea ikiwa imepita siku tatu tangu kutokea ajali ya gari aina ya Toyota Allion kuligonga Lori aina ya Mercedes Benz lililokuwa likivuta tela eneo la Iyovi lililopo Mikumi Barabara ya Morogoro kuelekea Mkoani Iringa na kuuwa watu watano.