Watu watano wamefariki dunia papo hapo baada ya kutokea kwa ajali ya gari ndogo aina ya Toyota Allion lenye namba za IT 6954 DNN iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Tunduma kugongana na Lori la mafuta aina ya Mercedes Benz lenye namba za usajili RAE 518 C lililokuwa likitokea Mkoani Iringa kuelekea Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoani Morogoro, Fortunatus Musilim amesema ajali hiyo iliyotokea majira ya usiku wa kuamkia Jumatatu Desemba 26, 2022 eneo la kona za Iyovi zilizopo Wilayani Kilosa Morogoro, katika barabara kuu ya Morogoro kuelekea Mkoani Iringa.
Amesema, ajali hiyo imesababishwa na uzembe wa Dereva wa gari dogo ambaye inasemekana alikuwa akiendesha kwa mwendo kasi hali liliyopelekea gari kumshinda katika kona na kuligonga Lori hilo la mafuta lililokuwa na tela lenye namba za usajili RL 2686 ambalo hata hivyo lilikuwa halijabeba mafuta.
Kamanda Muslim amewataja waliofariki katika jali hiyo kuwa ni pamoja na Dereva wa gari dogo Festo Eliuzima Shoo, Greyson Silla Ngogo (50), Janeth John Luvanda (40), Osward John Luvanda (42) na John Davis Haule (37) ambapo miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mt. Kizito Mikumi kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi.