Mwimbaji mahiri wa muziki wa bongo fleva Diamond Platnumz afunguka kwa mara ya kwanza kuhusu madai ya baadhi ya watu ambao wamekuwa wakimtaja kama mmoja wa wasanii wasiopenda maendeleo ya wenzie na hata kumtaja kuwa mwenye roho mbaya.
Kuelekea kwenye onyesho lake la mwisho wa mwaka linalotarajiwa kufanyika usiku Desemba 3, 2022, Diamond amefanya mahojiano maalum na kuweka bayana kuwa anafahamu wapo watu wenye kuamini kuwa ameshiriki kukwamisha jitihada na mipango ya baadhi ya wasanii kiasi cha wengine kumuona kama mtu asiyependa maendeleo ya wengine.
Jambo alilolikanusha kwa kuweka wazi uhalisia wa maisha yake na namna anavyopenda kushiriki katika kuhakikisha anaunga mkono jitihada za wasanii wengine.
“Mimi siamini kwamba mtu mwingine akifanikiwa ndio mimi nitafeli hapana, watu wakati mwingine naona wanaandika kwenye mtandao kwamba ninaroho mbaya, lakini sijawahi kuwa na roho mbaya.
Kwa sababu mimi naweza kusema ndio msanii ambaye nimetoa wasanii wengi wenye nguvu katika nchi, na sijawahi kuwa na tatizo na mtu, labda tu unaweza kusikia wachonganishi wakizungumza mambo ambayo baadae yanakuja kuwa chuki.
Na siku hizi ninasapoti kazi zao, napenda kushiriki, napenda kuona ifanikiwe kwa sababu naamini kwa namna moja au nyingine muziki ni maisha ya watu, ukifanikiwa mtu unakuwa umemkomboa kimaisha.” amesema Diamond.
Nyota huyo wa ‘Chitaki’ ameyasema hayo alipokuwa akifanya mahojiano na kituo cha Wasafi, baada ya kuulizwa kuhusu ushiriki wake katika kazi za wasanii wenzake wa nyumbani.
Aidha Diamond amewaondoa hofu mashabiki wake, kwa kuwaarifu kuwa afya yake kwa sasa ni njema na yuko tayari kuwaburudisha kwenye usiku wa onyesho la Cheers 2023 litakalofanyia Ramada Hotel jijini Dar es salaam.