Serikali inatekeleza mpango wa kuboresha huduma ya maji Jijini Mbeya kwa kufanya usanifu na kujenga mradi wa maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira, ili kuwahudumia wakazi 780,000.
Hayo, yamesemwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso katika ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ya kuzungumza na wananchi wa Mbeya Mjini eneo la Kambwe Stendi wakati akieleza mambo mbalimbali yanayohusiana na Sekta ya Maji.
Amesema, mahitaji halisi ya maji ni lita milioni 90 kwa siku dhidi ya uzalishaji wa sasa wa lita milioni 66.5 kwa siku, ambayo ni sawa na asilimia 74 ya mahitaji husika.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa mradi huo utazalisha Lita Milioni 117 kwa siku na umepangwa kutekelezwa katika kipindi cha miezi 24, huku taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi zikiwa zimekamilika na Mkataba unatarajiwa kusainiwa ndani ya Januari 2023.