Klabu ya Arsenal ya Jijini London imekamilisha usajili wa Mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji Leandro Trossard kwa ada ya pauni milioni 27, akitokea Brighton inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

Usajili wa Mshambuliaji huyo umekamilishwa, baada ya Trossard kufanyiwa vipimo vya afya jijini London jana Ijumaa, huku ikielezwa kuwa huenda akawa sehemu ya kikosi cha The Gunners kitakachoivaa Manchester United kesho Jumapili (Januari 22).

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 amesaini mkataba wa miaka minne na nusu, ambao una kipengele za kuongeza mwaka mmoja zaidi.

“Tuna furaha sana kuwa naye,” amesema meneja Arsenal Mikel Arteta katika mkutano wake na waandishi wa habari kuelekea mchezo dhidi ya Man Utd

“Ni mchezaji ambaye tumemfuatilia kwa muda sana, tuliona kuna uhumuhimu wa kumsajili katika kipindi hiki kwa sababu, tulihitaji kufanya hivyo.”

“Ni Mchezaji ambaye ana uwezo wa kucheza nafasi tofauti, anaijua ligi ya England, ana uzoefu na anaweza. Ninaamini ataingia kwenye mfumo wa timu kwa haraka zaidi.”

“Tunapaswa kufikiria muda mfupi lakini pia muda wa kati na mrefu. Anatupa yote hayo. Unapoangalia kazi yake na kile alichokifanya katika miaka michache iliyopita ni mchezaji anayelingana aina yetu ya uchezaji.”

Trossard ataungana tena na meneja wake wa zamani wa Genk ambaye ni Kocha msaidizi wa Arsenal Albert Stuivenberg huko kaskazini mwa London.

Wakati huohuo, akizungumzia timu ya wakufunzi ya Arsenal, Trossard aliiambia tovuti ya klabu: “Waliniambia wananipenda sana kama mchezaji, kwamba ningefaa sana mfumo na jinsi wanavyotaka kucheza.”

“Inanisaidia kuwa na uwezo wa kucheza katika nafasi tofauti. Wanatazamia kufanya kazi na mimi na kinyume chake. Ninafurahi sana kufanya kazi nao na nadhani Mikel [Arteta] ni kocha sahihi kwangu kwa sasa.”

“Huu umekuwa msimu wangu bora zaidi kwenye Ligi Kuu hadi sasa. Tulifanya kazi nzuri huko Brighton na kiwango changu kimekuwa kizuri sana. Ni wazi sijacheza sana tangu tulipomaliza Fainali za Kombe la Dunia, lakini ninafuraha sana kuanza mwaka 2023 nikiwa na Arsenal.”

Arsenal ilihamishia nguvu ya kumsajili kwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji baada ya kumkosa Mykhailo Mudryk, aliyejiunga na Chelsea akitoka Shakhtar Donetsk Januari 15.

Dani Alves apoteza kazi Mexico
UEFA yaingilia kati sakata la Juventus FC