Mshambuliaji kutoka nchini Zimbabwe Prince Dube amesema Azam FC itapambana vilivyo dhidi ya Singida Big Stars itakayokuwa nyumbani Uwanja wa Liti, mjini Singida.

Mchezo huo wa Mzunguuko wa 21 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, umepangwa kuchezwa Jumatatu (Januari 23), huku Azam FC ikisafiri kuelekea mkoani Singida tayari kwa mchezo huo.

Dube amesema wanatambua Azam FC ina deni la kulipa kisasi dhidi ya Singida Big Stars, baada ya kupoteza 4-1 katika Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023, kisiwani Unguja ‘Zanzibar’ mapema mwezi huu.

“Mabao 4-1 ni mengi sana baada ya mchezo sisi wenyewe tulijikuta tunashangaana, kwa sababu haikuwa rahisi kukubaliana na matokeo hayo, tumehimizana kuwa matokeo kama hayo yasijirudie tena tutakapokutana na Singida Big Stars kwenye mchezo wa Ligi Kuu.”

“Tunajua hautakuwa mchezo rahisi lakini kama wachezaji tumeshahimizana, tunakwenda kupambana ili kupata matokeo katika Uwanja wa ugenini,”

“Tunataka kuona kila mmoja anayeipenda Azam FC anakuwa na furaha baada ya mchezo wetu dhidi ya Singida Big Stars, pia tunahitaji kuendelea kujiimarisha katika nafasi za juu katika msimamo wa Ligi Kuu.” amesema Mshambuliaji huyo aliyefunga mabao matano msimu huu

Hata hivyo katika Duru la Kwanza la Ligi Kuu msimu huu, Azam FC ikicheza nyumbani Azam Complex Chamazi, jijini Dar es salaam ilishinda 1-0 dhidi ya Singida Big Stars, bao lao likifungwa na Kiungo Sospeter Bajana.

Wanawake, watoto waliotekwa waachiliwa huru
Sabilo akiri maji yamezidi unga Mbeya City