Takriban watu 20 wamefariki usiku wa kuamkia Januari 27, 2023 katikati mwa nchi ya Chad kutokana na mwendokasi wa basi walilokuwa wakisafiria, uliosababisha kugonga lori lililokuwa limeharibika na kuegeshwa njiani.
Taarifa ya Wizara ya uchukuzi imesema, ajali hiyo iliyojeruhi watu saba wawili wakiwa katika hali mbaya ilitokea katika eneo la jangwa lililopo kilomita 35 kutoka mji wa Oum-Hadjer na kilomita 500 mashariki mwa mji mkuu wa wa nchi hiyo, N’Djamena.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Basi hilo mali ya shirika la usafirishaji la N’Djamena lilikuwa likielekea mji wa Abéché uliopo jimbo la Ouaddaï, likiwa limebeba watu 31 ambapo watu 18 walifariki papo hapo na wawili hospitalini.
Ajali mbaya zinazohusisha mabasi, ambayo mara nyingi hujaa kupita kiasi na kuendeshwa kwa mwendo wa kasi, hutokea mara kwa mara katika barabara za Chad ambapo Februari 28, 2022, watu 33 walifariki na 54 kujeruhiwa baada ya mabasi mawili kugongana barabara ya N’Djamena-Abéché, karibu na mji wa na Oum-Hadjer.