Klabu ya Simba SC imetoa ufafanuzi wa kina kuhusu kuachwa kwa Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Burundi Saido Ntibazonkiza, kwenye safari ya Guinea.
Kikosi cha Simba SC kimeondoka jijini Dar es salaam mapema leo Alhamis (Februari 09) kuelekea Counakry-Guinea kupitia Addis Ababa-Ethiopia, tayari kwa mchezo wa kwanza wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Horoya AC.
Daktari wa Simba SC, Edwin Kagabo amesema Saido ameshindwa kuambatana na Wachezaji wenzake katika safari hiyo, kufuatia kukosa utimamu wa mwili, baada ya kukosa sehemu ya mazoezi kabla ya safari ya leo.
“Saido alipata maumivu ya nyama za paja katika mchezo dhidi ya Singida Big Stars, hali yake imeimarika lakini hawezi kusafiri kwa kuwa hayuko timamu na hajafanya mazoezi na wenzake. Timu ikirejea atajiunga na wenzake.” amesema Dk. Edwin.
Simba SC itacheza dhidi ya Horoya AC Jumamosi (Februari 11) katika Uwanja wa General Lansana Conte, saa moja usiku kwa saa za Tanzania.