Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), linatarajia kufanya mkutano wa Kawaida wa 43 jijini Bujumbura nchini Burundi Februari 23, 2023.
Mkutano huo. ambao umeanza kwa ngazi ya Wataalam Februari 19 – 20, 2023 utafuatiwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu utakaofanyika wa Februari 21 – 22, 2023 na kuhitimishwa na mkutano huo wa Mawaziri.
Agenda mbalimbali zinatarajia kujadiliwa kuhusu mtangamano wa Jumuiya hiyona baadaye zitawasilishwa kwenye Mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu kwa majadiliano kabla ya kuwasilishwa ngazi ya Mawaziri.
Miongoni mwa agenda hizo ni pamoja na taarifa ya Utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa kwenye vikao vilivyopita katika maeneo mbalimbali ikiwemo biashara na forodha, miundombinu, ulinzi na usalama, sheria, utalii, ajira na utawala na fedha.
Nyingine ni kupokea taarifa ya mwaka ya Ukaguzi wa Hesabu za Jumuiya kwa mwaka wa fedha ulioishia mwezi Juni 2022, taarifa ya Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya, Taarifa kuhusu Taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kupitia na kupitisha ratiba ya shughuli za Jumuiya kwa kipindi cha Januari – Juni 2023.