Serikali nchini, imemuagiza Kamishna wa Elimu kufanya uchunguzi wa kina kwa Shule nne zilizobainika kufanya udanganyifu mkubwa katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2022.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda wakati akizungumza na wazazi, walezi wa wanafunzi waliofutiwa matokeo ya mtihani wa kidato nne 2022 wa shule ya Sekondari Thaqaafa ya Jijini Mwanza kwa ajili ya kuwasikiliza.

Amezitaja shule hizo, kuwa ni Cornelius ya Kinondoni Dar es Salaam, Thaqaafa ya Mwanza, Mnemonic ya Zanzibar na Twibhoki iliyoko Mara na kumtaka Kamishna huyo kuchukua hatua kali kulingana na ripoti ya uchunguzi huo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima akizungumza katika kikao hicho.

Mkenda amesisitiza wazazi kuwalea watoto katika maadili ili watambue kuwa udanganyifu si mzuri na una madhara makubwa katika upande wa haki, maadili na uweledi.

“Tunapowapeleka watoto shule tunataka wajifunze waelewe ili baadae waje watumikie taifa. Sasa mtu anakuja kuwa daktari au mhandisi au rubani kwa kuiba mtihani, madhara yake ni makubwa sana,” ameongeza Mkenda.

Mkenda amewapa pole wazazi na kuwataarifu kuwa mitihani hiyo imefutwa na hivyo kilichopo ni kurudia mitihani.

Sehemu ya Wazazi walikuwa wamehudhuria kikao na Waziri wa Elimu.

“Kuhusu kurudia mtihani tumewasikiliza maombi yenu, ninashukuru kuwa hamna anayesema ameonewa sote tunakubaliana kuwa kulikuwa na udanganyifu na hivyo niseme matokeo yamefutwa na kikubwa ni maombi ya kurudia mtihani. Hili tunalichukua tutawasiliana nanyi baada ya kulifanyia kazi kwani ni suala la kibajeti pia,” amesema Mkenda.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amesema Serikali haitalea shule zinazofanya udanganyifu wa mitihani na kuongeza kuwa wanafunzi wanatakiwa wapimwe kwa uwezo na sio kwa kudanganya.

Mstaafu: Kenyatta aingilie kati mvutano Raila, Ruto
Mkutano Baraza la Mawaziri EAC kufanyika Bujumbura