Waendelezaji wa ujenzi wa mradi wa majengo mapya ya kisasa ya makazi katika eneo la Nungwi Mashariki mjini Zanzibar, wamewakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwenye mradi huo wenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 100 (zaidi ya 236bn/-).
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, ambayo imetolewa na waendelezaji wa mradi huo, Squid Limited Zanzibar, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, George Alexandru alieleza kuwa ujenzi wa mradi ulianza Desemba 2022 na kwamba awamu ya kwanza itakua na nyumba 238.
Amesema, kwa uwekezaji wa awali wa dola za Kimarekani 50,000 tu (118m/-), mwekezaji anaweza kuwa mmiliki wa mradi mkubwa wa The Ocean Pearl Zanzibar, unaotarajiwa kuwa wa aina yake visiwani baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza mwezi Januari 2025.
Mradi huo ambao umesajiliwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) na kuthibitishwa kuwa na thamani ya dola za Kimarekani milioni 105, unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36, na hauna ubaguzi kwa wawekezaji wa ndani na nje, ili kununua nyumba hizo za kifahari.
Kwa mujibu wa marekebisho namba 10 ya Zanzibar Condominium Act ya 2010, baada ya ununuzi uliofanikiwa, mnunuzi atapewa hati ya umiliki ya kukodisha kwa miaka 99. Muda wa kukodisha kwa kawaida hutolewa kwa awamu za miaka 33 kila moja.
Hata hivyo, amesema, kwa wale wanaowekeza katika mradi huo ya kifahari watanufaika ka punguzo la kodi kama wakazi na makadirio ya kupata faida ya uwekezaji ya asilimia 12 kila mwaka huku malipo ya faida yakitegemewa kuanza kupatikana baada ya miaka saba, kwa mujibu wa mwendelezaji wa mradi huo.
“Baada ya kuwekeza katika The Ocean Pearl Zanzibar, iwe kwenye majengo ya studio, duplex au villa zakifahari, mwekezaji ana hiari ya kuikodisha kama nyumba ya mapumziko ya sikukuu au likizo au makazi ambayo itasimamiwa na kampuni mahususi ya kutoa huduma za ukarimu,” alisema Mkurugenzi huyo.
Mradi huo pia unatoa huduma za fukwe za bahari, chakula, na safari kwenye visiwa vya karibu, historia na utamaduni ukiwa na hadhi ya nyota tano na utakuwa na huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na migahawa, baa pamoja na baa kwenye gati, klabu ya usiku, dukai, eneo la mazoezi, na mabwawa ya kuogelea.
Awamu ya kwanza ya mradi huo, inajengwa kwenye eneo la zaidi ya mita za mraba 130,000 itakayojumuisha kituo cha biashara wakati eneo kubwa litakuwa maalum kwa mabwawa ya kawaida na bustani huku ujenzi wa eneo la kutua helikopta unatarajiwa kuwezesha kufikika kwa anga, aliongeza.