Mwanaume aliyeonekana katika Picha za kamera ya kificho akigongwa na Basi liendalo haraka eneo la kisutu jijini Dar es salaam jana, amelazwa na anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, chumba cha wagonjwa mahututi ICU.
Akithibitisha uwepo wa taarifa hizo, Meneja wa Kitengo cha Uhusiano, Taasisi ya tiba ya mifupa Hospitali ya Muhimbili – MOI, Patrick Mvungi amesema majeruhi huyo jina na taarifa zake bado hazijajulikana.
Amesema, katika ajali hiyo, Mwanaume huyo alivunjika mguu, mkono na kuumia kichwa na kwamba bado hawezi kuongea ingawa anafungua macho, na jana (Februari 22, 2023), Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano Neema Mwangomo alisema hakuna kifo.
Basi hilo la mwendokasi lililokuwa linatokea Kivukoni lilipata ajali ya kugongana na gari dogo aina ya Toyota Rav4 eneo la Kisutu, watu 37 walijeruhiwa wakiwemo Wanafunzi 24 na Watu wazima 13 ambao wengi wao waliruhusiwa baada ya kupata matibabu.