Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amewakaribisha wawekezaji kutoka Umoja wa Ulaya kuwekeza nchini katika sekta za Kilimo, Usafirishaji, Nishati,Tehama,Utalii na katika Viwanda vya kuongeza thamani kwa kuwa serikali inahitaji kufungua zaidi sekta hizo ili kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Makamu wa Rais amesema hayo hii leo Februari 23, 2023 wakati akifungua Jukwaa la Kwanza la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, linalofanyika Jijini Dar es salaam na kusema Tanzania imedhamiria kuvutia uwekezaji katika kutumia rasilimali zilizopo kwa kuzingatia eneo la kimkakati ambalo ni fursa kiusalama wa chakula na ukuzaji wa kilimo.
Ameongeza kwamba kwa sasa Tanzania ipo katika maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa kwa miaka mingine 25 ambayo inalenga kubadilisha uchumi wa Taifa kutoka katika hali ya uchumi
wa kati wa chini hadi kufikia uchumi wa kati wa juu ambapo kwa kiasi kikubwa unahitaji biashara na uwekezaji.
Aidha, Makamu wa Rais pia amewahakikishia wawekezaji mazingira mazuri na salama ya uwekezaji na biashara hapa nchini kwa kuzingatia juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini.
Suala hilo litakwenda sambamba na kuweka sera imara na zinazotabirika pamoja nasheria na taratibu rafiki, kuboresha huduma za kijamii, kuimarisha demokrasia, usawa wa kijinsia na utawala wa sheria, kuendeleza miradi mikubwa ikiwemo ya nishati na miundombinu, uchukuzi na usafirishaji.
Aidha, Makamu wa Rais pia ametoa wito kwa Jukwaa hilo kuwa mwanzo wa mengine mengi yajayo na kuwa na mijadala ya wazi juu ya fursa, hofu na vikwazo vinavyozuia maendeleo ya haraka katika kuchochea uwekezaji na biashara baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya.