Ili kuhakikisha lengo la mchango wa sekta ya madini unafikia asilimia 10 ya pato ghafi la Taifa mwaka 2025, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), imeahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali huku ikimpongeza Rais Dkt. Samia kwa kuweka mazingira wezeshi ya sekta hiyo ambapo kwa sasa imefikia asilimia 9.2
Kauli hiyo imetolewa na Makamu Rais wa GGML, AngloGold Ashati anayeshughulikia miradi endelevu nchini Ghana na Tanzania, Simon Shayo wakati akizungumza kwa niaba ya wadau wa sekta ya madini kwenye mdahalo wa miaka miwili ya Rais Samia madarakani.
Amesema, ripoti za karibuni kutoka Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta, na Gesi Asilia (TEITI), zinaonesha GGML inachangia kati ya asilimia 30 na 40 ya mapato yote ya dhahabu inayouzwa kwa sekta ya madini Tanzania na kwamba wanaamini wanaweza kuvuka lengo lililowekwa na Serikali iwapo wawekezaji pamoja na wachimbaji wadogo wataendelea kujengewa mazingira bora ya uwekezaji.
“Tunaendelea kuiomba serikali chinIi ya uongozi wa Rais Samia kuendelea kutuwekea mazingira mazuri, tunaahidi kuongeza tija kwenye migodi yetu na sisi AngloGold Ashanti kupitia mgodi wetu wa GGML tunaamini wakati wote tutaendelea kuwa sehemu kubwa ya mafanikio hayo ya sekta ya madini,” alisema Shayo.
Aidha ameongeza kuwa, “uwajibikaji wetu kwa jamii kupitia mpango ambao unasainiwa kwa pamoja tangu mwaka 2017, tumewekeza kila mwaka kati ya Sh bilioni 9.2. hadi 9.5 na mwaka huu tunaamini tutapata fursa ya kuunganisha mipango miwili ya mwaka 2022 na 2023 ambapo kwa wilaya ya Geita peke yake tutawekeza kiasi cha Sh bilioni 18.4.”
Awali, akizungumza katika mdahalo huo Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigela alisema mkoa huo ndio namba moja kwa uzalishaji wa madini ya dhahabu kwani asilimia 60 ya mapato ya Taifa inatoka kwenye madini na kwamba miaka miwili iliyopita, wachimbaji wadogo na wakati walizalisha kilo 13,000 sawa na tani 13.5 wakati migodi mikubwa kama GGML ilizalisha kilo 35,000 sawa na tani 35.