Mahakama ya Wilaya Tunduru mkoani Ruvuma, imemhukumu Mohamed Ngwelekwe (25) mkazi wa kijiji cha Namiungo, wilayani humo, kutumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumnajisi mtoto wake wa kiume wa kumzaa mwenye umri wa miaka minne.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Honorius Kando ambaye alisema, mtuhumiwa alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti katika kijiji hicho.

Kando alisema mtuhumiwa ametenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 158 kifungu kidogo cha(1)(a) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Awali, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mtoto huyo ambaye jina lake limehifadhiwa alieleza kuwa kila alipokuwa anakataa kufanyiwa kitendo hicho ,baba yake alikuwa anamng’ata na kumpiga sehemu za mwili wake na kumtishia.

Daktari aliyemfanyia uchunguzi mtoto huyo, aliiambia Mahakama kuwa uchunguzi wa kitabibu umebaini ni kweli mtoto huyo alifanyiwa vitendo hivyo vya kinyama.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro, alipongeza jeshi la polisi wilayani humo kupitia kitengo cha cha Dawati la Jinsia kwa jitihada walizofanya tangu serikali ilipopata taarifa hizo.

Mtatiro alisema, mtoto huyo amefanyiwa kitendo hicho kwa muda mrefu na kuwaasa wananchi popote walipo kutoa taarifa serikalini kila wanapobaini kuwepo kwa vitendo vya aina hiyo ambavyo ni kinyume na maadili na vina hatarisha ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.

Bianchi: Tumekuja kulipa kisasi
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Machi 6, 2023