Waandishi wa Habari na Wachambuzi wa michezo nchini Tanzania wameaswa kuacha kushadadia sakata la Kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum ‘Fei Toto’, ambaye yupo kwenye mzozo wa kuvunja mkataba na Klabu ya Young Africans.

Sakata la Kiungo huyo limekwama kwa mara mbili mfululizo mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, ambayo imesisitiza Fei Toto bado ni mchezaji halali wa Young Africans kwa mujibu wa mkataba uliopo baina ya pande hizo mbili.

Akizungumza na baadhi ya Waandishi wa Habari mapema leo Jumatatu (Machi 06) katika Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ Jasmin Razack ambaye amewahi kuwasaidia Wachezaji mbalimbali kwenye migogoro ya kimkataba na Club zao akiwemo Simon Msuva, Wilfred Bony aliyewahi kucheza Man City na Swansea na Emmanuel Eboue aliyewahi kucheza Arsenal, amesema haipendezi kuona na kusikia Sakata la Feisal likizungumzwa kwa kuponda ama kushadadia.

“Waandishi msikurupuke kwenye kusema Feisal kaonewa ama ameshindwa maneno mengi tuwe na uzalendo, ninaomba tuvute subra kwa mara ya kwanza leo Feisal kaleta ombi lake naimani kama litashughulikiwa nina imani na TFF, chombo pekee kinachoweza kuvunja mkataba wa mchezaji ni TFF” amesema Jasmin Razack

Feisal Salum leo Jumatatu (Machi 06) alifika kwenye Ofisi za TFF Dar es salaam kuwasilisha ombi kulitaka Shirikisho hilo kuuvunja mkataba wake na Young Africans ikiwa ni siku chache zimepita tangu shauri lake litupiliwe mbali na Kamati ya Sheria na HAdhi za Wachezaji.

Feisal alifika Makao Makuu ya TFF akiwa ameongozana na Mwakilishi wake Jasmin Razack wakiwa na barua mpya ya kuomba kuvunja mkataba wake na Young Africans.

Moses Phiri aichimba mkwara Vipers SC
Pato ghafi la Taifa: GGML yamtaja Rais Samia