Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limeweka hadharani zawadi kwa Bingwa wa Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu 2022/23.
Zawadi kwa Bingwa wa Michuano hiyo imewekwa wazi, huku Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ikiwa katika hatua ya Makundi Mzunguuko wanne ambao rasmi utaanza kuchezwa leo Jumanne (Machi 07) katika viwanja mbalimbali Barani humo.
Taarifa ya CAF imeelezwa kuwa Bingwa wa Michuano hiyo msimu huu 2022/23 atanyakuwa kiasi cha Dola za Marekani Milioni 2.5 (sawa na Shilingi 5,830,125,000,000 za Kitanzania).
Mshindi wa Pili wa Michuano hiyo atapata Dola za Marekani Milioni 1.25 (sawa na Shilingi 2,915,062,500,000 za Kitanzania), huku timu zitakazofika Hatua ya Nusu Fainali zikitarajia kuvuna Dola za Marekani 800,000 (sawa na Shilingi 1,865,640,000 za Kitanzania).
Timu zitakazotinga Hatua ya Robo Fainali zitazawadiwa Dola za Marekani 650,000 (sawa na Shilingi 1,515,832,500 za Kitanzania), huku Timu zitakazomaliza nafasi ya tatu na nne katika hatua ya makundi, zitaondoka na Dola za Marekani 550,000 (sawa na Shilingi 1,282,627,500 za Kitanzania).
Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika Bingwa atazawadiwa Dola za Marekani Milioni 1.25 (sawa na Shilingi 2,915,062,500,000 za Kitanzania).
Mshindi wa pili atachukua Dola za Marekani 625,000 (sawa na Shilingi 1,457,531,250 za Kitanzania) na Nusu Fainali Dola za Marekani 450,000 (sawa na Shilingi 1,049,422,500 za Kitanzania).
Robo Fainali Dola za Marekani 350,000 (sawa na Shilingi 816,217,500 za Kitanzania), nafasi ya tatu na nne hatua ya makundi Dola za Marekani 275,000 (sawa na Shilingi 641,313,750 za Kitanzania).
Ni wazi klabu za Tanzania Simba SC inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Young Africans inayoshiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika, zina nafasi ya maamuzi ya kuchukua moja ya zawadi hizo zilizotangazwa na CAF.
Simba yenye alama 03 katika Kundi C, Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa nafasi ya tatu, leo Jumanne (Machi 07) inatarajiwa kujitupa Uwanja wa Mkapa, Dar es salaam, kuivaana na Vipers SC ya Uganda.
Kesho Jumatano (Machi 07), Young Africans iliyo nafasi ya pili Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika, kwa kukusanya alama 04, itakuwa inakabiliana na AS Real Bamako ya Mali kwenye Uwanja wa Mkapa.