Uongozi wa Young Africans umeendelea kusisitiza kufuatwa kwa utaratibu wa kuvunjwa kwa Mkataba kati yao na Kiungo kutoka Visiwani Zanzibar Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’.

Tayari Klabu hiyo imethibitisha kupokea hukumu ya maamuzi ya marejeo ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuhusu suala la kiungo huyo, ambaye hakuridhishwa na maamuzi ya awali yaliyotolewa mwezi Januari 2023 na Kamati hiyo.

Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe amesema hakuna anayemzuia Feisal Kuondoka klabuni hapo, na amawataka Wadau wa Soka kufahamu hilo, lakini msimamo wa Klabu hiyo ni kuhakikisha mchezaji huyo anaondoka kwa utaratibu.

Amesema kuna dhana ambayo imejengeka kwa baadhi ya Wadau wa Soka wakidhani Young Africans inamfanyia kusudi Feisal, lakini ukweli ni kwamba kinachofanyika ni kusimamiwa kwa Kanuni za uhamisho ama kuvunjwa kwa Mkataba wake.

“Hatumzuii Feisal alum kuondoka, lakini utaratibu unapaswa kufuatwa. Timu inayomtaka ije Jangwani tuzungumze milango iko wazi na tuache kona kona.”

“Kila siku kuweka vikao visivyoisha havina maana kwa sasa. Atakama kuna timu imevutiwa na utendaji wa Rais wetu Hersi Said nayo ije tuzungumze, maana kuna timu nyingine zinamtamani.” amesema Ally Kamwe

Mwishoni mwa mwaka 2022 Feisal Salum aliandika katika ukurasa wake wa Instagram kuhusu kuvunja mkataba wake na klabu ya Young Africans, hali ambayo ilisababisha kuzuka kwa sakata la kufikishwa mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF mapema mwezi Januari 2023, kabla ya mtuhumiwa kuomba kurejewa kwa hukumu hiyo mapema mwezi Machi.

Sarakasi Bungeni imelipa: Massay kujengewa Barabara ya lami
Siku ya Wanawake Duniani: REA yatoa Majiko Banifu 114