Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Namibia zimesisitiza kuweka mikakati imara ya ushirikiano itakayoimarisha mfumo wa utendaji kazi, kwa lengo la kukuza na kuendeleza Diplomasia ya uchumi kwa maslahi ya nchi hizo pamoja na watu wake.
Msisitizo huo, umetolewa katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano – JCC, kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Namibia unaofanyika Jijini Windhoek, Namibia Machi 8 – 10, 2023.
Akifungua mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amesema Tanzania itaendelea kuweka mikakati imara ya ushirikiano na kukuza uchumi kati yake na Namibia, ili kuuenzi ushirikiano huo wa kihistoria.
“Ni matumaini yangu mkutano huu utatuwezesha kusaini makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya anga ili kurahisisha uwepo wa safari za moja kwa moja baina ya nchi zetu na kuwezesha uendeshaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wetu,” alisema Balozi Fatma.
Aidha, Balozi Fatma ameongeza kuwa ushirikiano huo uliasisiwa tangu enzi za harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika na waasisi wa mataifa hayo mawili, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mwl. Julius Nyerere, na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Namibia, Hayati Dkt. Samuel Nujoma.
Tanzania na Namibia, zinashirikiana katika sekta za Diplomasia, Siasa, Ulinzi, Uvuvi na Rasiliamali za Bahari, Kilimo, Maji, Maendeleo ya Miji, Madini, Nishati, Biashara, Uwekezaji, Mazingira, Utalii na Maliasili, usafiri, Afya, Utamaduni na Elimu.