Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema alipopata mwaliko wa kuwa Mgeni rasmi kwenye Kongamano la Siku ya Wanawake lililoandaliwa na Wanawake wa CHADEMA hakukataa kwasababu Wanawake hao ni kundi lake pia kwakuwa yeye ni Rais wa Watanzania wote bila kujali itikadi za Vyama.

Akiwa Mjini Moshi kwenye kongamano hilo Rais Samia amesema “Leo tunaandika historia mpya katika jitihada za kuendelea kuimarisha Taifa letu, niwapongeze Wanaume waliopo hapa ndani mnajua pekee yetu Wanawake hatuwezi lazima Wanaume muwepo, nimefurahi namuona Mwanangu Wenje yupo hapa kanawiri, na Mwanangu Lema yupo hapa, karibuni Tanzania hii ndio Tanzania njema.”

“Nilipopata mwaliko kuja kuwa Mgeni rasmi sikusita kwasababu nikiwa Rais wa Tanzania kundi hili ni kundi langu pia, huwezi kuitwa na Wananchi wako ukasema siji lakini nilifurahi kuja kwasababu nitajua leo Wanawake wa CHADEMA wanasema nini na nimesikia”

“Lengo letu ni kuona Mwanamke anathaminiwa na kupewa haki, nataka niwaambie tuliyoyazungumza hapa bei zimepanda, sijui chakula kina nini, afya bora ni kila Mwanamke wa Tanzania anapata hizo changamoto maana changamoto hazichagui Dini, Kabila wala rangi.“

“Kama tunakung’utwa huko majumbani wote tunakung’utwa , kama tunasukumwa visogo wote tunasukumwa, kama Wababa wana michepuko nyumba zote zina michepuko uongo Ndugu zangu?, kama kuna kuzodoana baina ya Mawifi na Wakwe ni wote Wanawake wa Tanzania”

“La kufanya sasa, nimesikia hapa mnaimba ‘Peoples Power’ yaani nguvu ya Watu, ile nguvu ya Watu ya Wanawake wa CHADEMA ikaungane na kila Mwanamke wa Chama chochote tukamkomboe Mwanamke, tuungane tuyatatue yale tuliyoyalilia hapa.”

Rais waogope chawa ni wanafiki, waongo: Mbowe
Wanaompinga Rais Katiba mpya wanampima: BAWACHA