Wakati Kikosi cha Simba SC kikitarajiwa kushuka dimbani Usiku wa kuamkia kesho Jumamosi (April Mosi) katika mchezo wake wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi Raja Casablanca, kocha wa timu hiyo Roberto Oliveira Robertinho’, ametamba kuwa watahakikisha wanashinda mchezo huo ili kuweka heshima.
Simba SC itashuka dimbani kuivaa Raja Casablanca saa 7:00 kwa saa za Tanzania sawa na saa 4:00 usiku kwa saa za Morocco, katika Uwanja Mohemmed V, mjini Casablanca.
Mchezo huo unaotarajiwa kuwa upinzani mkubwa huku Simba SC ikitarajiwa kuingia uwanjani kuvaana na Raja Casablanca ikiwa na hasira za kutoka kufungwa mabao 3-0 walipocheza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo Simba SC itashuka dimbani huku ikiwa tayari imefuzu hatua ya Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika pamoja na Raja Casablanca.
Akiwa katika Mkutano na Waandishi wa Habari kuelekea mchezo huo, kocha Robero Oliviera ‘Robertinho’ amesema atahakikisha anawajenga wachezaji wake kisaikolojia waweze kupambana na kuweka heshima kwa kushinda.
“Utakuwa mchezo mgumu kwetu lakini tunahitaji, Raja ni timu bora na hasa sisi tunaenda kucheza katika uwanja wa ugenini lakini hatutakubali kuona tunapoteza mchezo huo,” amesema Robertinho
Naye Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi chao kimefika salama Morocco na mwalimu maandalizi ya mapema kwa ajili ya mchezo huo.
Amesema timu yao ilichelewa kufika nchini humo kutokana na kupata hitirafu ya ndege lakini kocha Robertinho, amesema atapambana kuhakikisha wanashinda mchezo huo.
Ahmed amesema baada ya kumalizika kwa mchezo huo, timu itapumzika siku moja na Jumapili saa 7:00 mchana kikosi kitatua Dar es Salaam.
Simba ilifanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kuicharaza mabao 7-0 Hoyora FC katika mchezo wake uliochezwa uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo, umeifanya kufikisha alama tisa nyuma ya vinara Raja Casablanca ya Morocco iliyokuwa ya kwanza kutinga Robo Fainali katika kundi ‘C’ kufuatia kufikisha alama zake 13.