Kikosi cha Azam FC kimeondoka jijini Dar es salaam mapema leo Ijumaa (Mei 05) kuelekea mkoani Mtwara, tayari kwa mchezo wa Nusu Fainali wa Kombe la Shirikisho la Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Simba SC.
Mpambano huo, umepangwa kufanyika keshokutwa Jumapili (Mei 07) katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara kuanzia saa 9.30 alasiri.
Kabla ya kuondoka jijini Dar es salaam, Kocha Mkuu wa timu hiyo Kali Ongala, amesema kikosi chake kimejipanga vizuri kuhakikisha kinatinga hatua ya Fainali ya mashindano hayo kwa kuwafunga Simba SC.
“Najua Simba nao wanalitolea macho kombe hilo, ila sisi tunalihitaji zaidi, tunapata kuhakikisha mazuri katika mchezo huo muhimu, nia yetu kubwa ni kutinga fainali na kutwaa taji na tupate nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa, msimu ujao,” amesema Kocha huyo
Katika hatua nyingine Afisa Habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe, amesema kikosi chao kipo tayari kupambana na Simba SC na kutokana na maandalizi makubwa waliyoyafanya wanaamini watapata ushindi katika mchezo huo.
“Tunajua Simba SC imetoka kutolewa kimataifa hivyo, hasira zao zote wanataka kumalizia katika mchezo huu, niwaambie tumejipanga vizuri na wachezaji wote wana morari ya kutosha kuweza kushinda mchezo huo muhimu,” amesema lbwe.
Azam FC ilitinga Nusu Fainali kwa kuitoa Mtibwa Sugar iliyokubali kichapo cha mabao 2-0 katika mpambano uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam, huku Simba SC ikifanikiwa kuitoa timu ya Ihefu FC kwa kuifunga mabao 5-1.