Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema Serikali itagharamia mazishi ya Wanafunzi wawili (2) wa shule ya sekondari Mpalanga Wilayani Bahi waliofariki katika ajali ya gari iliyotokea jana majira ya saa 5:00 asubuhi katika Kijiji cha Chidilo Wilayani humo.

Aidha, Mhe. Senyamule ameahidi kuwa, Serikali itagharamia matibabu ya Wanafunzi wote majeruhi 31 walioumia katika ajali hiyo ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Ajali hiyo imehusisha gari yenye namba za usajili T 519 BSY aina ya Mitsubishi Canter mali ya Abdul Rashid mkazi wa Dar es Salaam na ilikuwa imebeba wanafunzi 51, walimu wawili na dereva mmoja ambao walikuwa wakielekea Shule ya Sekondari Magaga kushiriki mashindano ya michezo ya UMISETA.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Usalama barabarani Wilaya ya Bahi, ASP Bakari Ramadhani amesema kuwa, chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari hilo lililobeba wanafunzi, uliosababisha gari kumshinda dereva, kuacha njia na kupinduka na hadi sasa dereva wa gari hiyo anashikiliwa na jeshi la polisi.

Akitoa salamu za Serikali, Senyamule amewataka wafiwa kuwa na moyo wa subra na kuelekeza Jeshi la Polisi kuchukua hatua haraka kwa wote watakaothibitika kuhusika na uzembe huku akisema ameguswa sana na misiba hiyo ya kupoteza nguvu kazi ya Taifa la leo na kesho.

“Serikali iko pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu, tutaendelea kushirikiana katika wakati huu wa msiba kwa kusimamia mazishi ya marehemu na matibabu ya majeruhi wetu. Viongozi wote wakuu pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mwenye dhamana ya kusimamia Shule na Michezo mashuleni wanatoa pole sana,” amesema Senyamule.

Awali Senyamule aliwatembelea majeruhi 31 wanaoendelea na matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma huku Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dkt. Ernest Ibenzi akithibitisha kuendelea kuimarika kwa afya za majeruhi hao.

Pia, alizitembelea familia zilizopatwa na misiba hiyo katika Kijiji cha Nholi na Chidilo huku waliofariki wakitajwa kuwa ni Magreth Juma Shimba (18) mwanafunzi wa Kidato cha Nne ambae anatarajiwa kusafirishwa leo kuelekea Wilaya ya Kishapu, Shinyanga na Neema Yohana Hoya (16) mwanafunzi wa kidato cha pili atakaezikwa leo Kijiji cha Chidilo, Wilayani Bahi.

Real Madrid kuvunja rekodi ya usajili
Dodoma Jiji yakataa kuwa ngazi ya Ubingwa