Katika kesi hiyo namba 220 ya mwaka 2018, Membe alimdai Musiba fidia ya Sh10.3 bilioni kwa madai ya kumkashfu kupitia magazeti yake ya Tanzanite, ambapo Oktoba 28, 2021, Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam ilimuamuru Musiba kumlipa Membe fidia ya Shilingi 6 bilioni.
Wakili Mndeme amesema madai dhidi ya Musiba hayatafutika kwa sababu msimamizi wa mirathi ataendelea kufuatilia madeni ya marehemu na kwamba katika makosa ya jinai, mtuhumiwa akifariki kesi huisha lakini si kwa kesi ya madai.
Amesema kesi iko katika hatua ya kukazia hukumu au utekelezaji wa hukumu na maombi yaliwasilishwa mwaka 2022 na kupewa namba 26 ya mwaka 2022 na Mahakama ya Kuu Dar es Salaam, huku akimuelezea mteja kwamba alikuwa mtu anayepokea ushauri.
Membe alikuwa ni Waziri wa Mambo ya nje katika Serikali ya awamu ya nne, na amefariki Ijumaa Mei 12, 2023 katika Hospitali ya Kairuki iliyopo Mkoani Dar es Salaam wakati akipatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla.