Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inajipanga kupita kwenye maeneo yote yenye migogoro, ili kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kulinda maeneo ya hifadhi.

Majaliwa ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara ambaye alitaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kukomesha migogoro kwenye maeneo yaliyo jirani na hifadhi za Serikali.

Amesema, Serikali ilishaanza kulifanyia kazi suala la mgororo wa Tarime kwa kuunda timu ya Mawaziri wa Ardhi, TAMISEMI na Maliasili na Utalii ambao aliwapa maelekezo ya kwenda kukutana na wananchi wa Tarime.

“Timu hiyo ya Mawaziri imefanya kazi na inakamilisha taarifa yao. Wataileta kwangu, tutaipitia na kisha tutakwenda kwa pamoja kuelimisha wanavijiji. “Sisi ndani ya Serikali tunaamini kuwa wananchi wanaoishi jirani na hifadhi ni walinzi wa kwanza wa hifadhi zetu,” amesema.

Aidha ameongeza kuwa, mkakati wa Serikali wa kukomesha migogoro hiyo ni kushirikisha wananchi wa maeneo yote ambako migogoro hiyo inatokea na kufanya mapitio ya pamoja ili kubaini mipaka inapita wapi na tayari Serikali ilitoa maagizo kwa Mamlaka za Hifadhi ziweke vigingi virefu kwenye mipaka na vipakwe rangi nyeupe ili viweze kuonekana kwa urahisi.

Muujiza: Vichanga vyakutwa vikielea juu ya maji, vyaokolewa
Dkt. Kikwete ateta na Ban Ki-moon