Mwamuzi kutoka nchini Libya Ibrahim Mutaz ametajwa kuwa Mwamuzi wa mchezo wa Mkondo wa Pili wa Nusu Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini dhidi ya Young Africans ya Tanzania.

Mutaz amekabidhiwa jukumu hilo, huku Young Africans ikiwa mbele kwa mabao 2-0, na itahitaji matokeo ya sare ama ushindi wa aina yoyote, ili kujihakikishia safari ya kwenda kucheza Fainali ya Michuano hiyo.

Hata hivyo Mwamuzi huyo mwenye miaka 33, alipata beji ya uamuzi ya Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ kwa mara ya kwanza 2019, ameonekana kuwa na bahati na timu zinazokuwa nyumbani katika mashindano ya klabu Afrika kwani hakuna timu yoyote iliyowahi kupoteza mechi pindi anaposhika filimbi.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Mutaz amechezesha mechi 11 za mashindano ya klabu na kati ya hizo, timu zilizokuwa nyumbani zilipata ushindi mara sita na mara tano ilikuwa sare.

Ni mwamuzi asiyependa mzaha kwa wachezaji wanaocheza rafu na watovu wa nidhamu kwani katika mechi hizo 11, ametoa kadi 47 ikiwa ni wastani wa angalau kadi nne kwa mchezo, kati ya hizo, kadi 44 ni za njano na kadi nyekundu tatu.

Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limempanga Mutaz asaidiwe na Mlibya mwenzake, Attia Essa Amsaad na Mtunisia Khalil Hassan na refa wa akiba ni Mehrez Malki kutoka Tunisia.

Serikali kuwatua mzigo wananchi gharama za matibabu
Young Africans yajizatiti Afrika Kusini