Ripoti ya ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini DRC MONUSCO, inasema raia wapatao 500 waliuawa na Zaidi ya wengine milioni moja walikimbia makazi yao katika maeneo ya Djugu na Mahagi huko Ituri, kufuatia mashambulio ya makundi mawili ya wapiganaji wenye silaha.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyochapishwa na Mkuu wa MONUSCO mkoani Ituri kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Marc Karna Soro ni watu 500 wameuawa kati ya mwezi Desemba mwaka jana na Februari 2023.
Wengine ni karibia watu milioni moja, waliolazimika kuyahama makazi yao na kupewa hifadhi karibu na vituo mbalimbali vya kijeshi vya umoja wa mataifa, MONUSCO.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari jijini Bunia, Soro amesema mauaji hayo yalifanyika katika maeneo ya Tchabi, Boga na viunga vya wilaya mbili za Djugu na Mahagi, ambako waasi wa ADF pia wanaendeleza mauaji ya raia wa kawaida.