Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amehitimisha ziara yake ya siku nne Doha, Qatar, kwa kuzungumza na baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini humo maarufu kama wana-diaspora.
Ziara yake ambayo alikuwa akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa tatu wa Jukwaa la Uchumi Qatar, ilijumuisha mazungumzo na viongozi wa Qatar, kusaini makubaliano muhimu, kuhudhuria Jukwaa la Kimataifa la tatu la Uchumi.
Katika mkutano huo, Dkt. Mwinyi alijibu hoja mbalimbali zilizoulizwa na wana-diaspora hao ikiwemo ufafanuzi juu ya sera ya uchumi wa Buluu, Wanafunzi kupatiwa nafasi kusoma Qatar, Uraia kwa watoto wanaozaliwa nje ya nchi na wazazi wawili Watanzania na suala la kodi wanazotozwa kwa biashara zao zilizopo Tanzania.
Dkt. Mwinyi alizitolea ufafanuzi hoja hizo huku nyingine zikijibiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk, Balozi Mahadhi, Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA, Shariff A Shariff na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Gelead Teri.