Wakati Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera akitangaza kiingilio bure katika mchezo wa marudiano wa ‘Play Off’ Ligi ya Championship kati ya Mbeya City dhidi ya Mashujaa, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amejibu mapigo akitangaza dau nono kwa kila bao kwa kikosi cha Mashujaa.

Homera amesema shabiki anachotakiwa ni kufika uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mapema siku ya mchezo na kuisapoti timu hiyo kwa dakika zote 90 ili Mbeya City ibaki Ligi Kuu.

Mwenyekiti wa Mashujaa, Abdul Tika amesema katika kuongeza hamasa, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Andengenye amenunua kila bao litakalofungwa na vijana wake kwa Sh600,000.

Amesema kiongozi huyo amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Kigoma inapata timu ya Ligi Kuu ndio maana hata katika mchezo wa kwanza alinunu tiketi zote ili wapenzi wa soka wapate nafasi ya kuisapoti timu yao.

Mashujaa tayari imetanguliza mguu mmoja Ligi Kuu baada ya ushindi wa mabao 3-1 iliyopata Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, huku ikisaka sare au kutokufungwa bao zaidi ya moja ili kupata nafasi hiyo.

Tayari kikosi cha Mashujaa kimeshawasili jijini Mbeya kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa mwisho hatua ya mtoano dhidi ya Mbeya City utakaofanyika Jumamosi (Juni 24) kwenye Uwanja wa Sokoine.

“Maandalizi yapo vyema na tumejipanga kukabiliana na lolote katika hatua hii sababu tulikotoka ni mbali na tunakokwenda kunaonekana karibu japo kuna kazi ya ziada.

“Kamati ya hamasa inatarajia kuondoka Kigoma Ijumaa na mashabiki zaidi ya 200 na wengine watatoka Dar es Salaam ili kwenda kuisapoti timu yao Mbeya,” amesema Tika.

Mwenyekiti wa hamasa wa kikosi hicho, Abdul Singso amesema wamedhamiria kuisapoti timu yao hadi dakika ya mwisho ili kutimiza lengo lao.

Mashujaa imefika hatua hiyo baada ya kumaliza Ligi ya Championship nafasi ya nne kwa pointi 49 na kukutana na Pamba katika hatua ya kwanza ya mtoano, mchezo wa kwanza ilishinda 4-0 nyumbani na ugenini kupoteza 4-1.

Kocha msaidizi wa Mashujaa, Rashidi Idd ‘Chama’ amesema wamesafiri na wachezaji wote na wamefika salama wakiwa katika morali kubwa ya mchezo.

Hakuna wa kukuondolea changamoto, pambana - Kasesela
Lamin Jarjou kusajiliwa jumla jumla Azam FC