Mshambuliaji na Nahodha wa Timu ya Taifa ya Senegal Sadio Mane amethibitisha kuwa atabaki na Mabingwa wa Soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, licha ya klabu hiyo kuonyesha nia ya kumsajili Harry Kane.
Tottenham wamekataa dau la kwanza la Bayern la pauni milioni 70 kwa ajili ya kumnunua Kane, ambaye atafikisha miaka 30 mwezi ujao, lakini mabingwa hao wa Bundesliga wanatarajiwa kuwasilisha ofa ya pili hivi karibuni.
Mane mwenye umri wa miaka 31, amekuwa na wakati mgumu tangu ajiunge na Bayern akitokea Liverpool mwaka mmoja uliopita, kutokana na jeraha la mguu ambalo lilimweka nje kwa muda mrefu na akakosa fainali za Kombe la Dunia Qatar, mchezaji huyo wa kimataifa wa Senegal amefunga mabao saba katika mechi 25 alizocheza Bundesliga.
Mane alipamba vichwa vya habari kufuatia ugomvi kati yake na mchezaji mwenzake Leroy Sane na akasimamishwa kazi na kutozwa faini.
Mane aliulizwa na mtangazaji wa Senegal 2sTV kama ataendelea kukipiga Bayern, Mane alisema: “Ndiyo, Mungu akipenda. Endapo mambo yataenda sawa nitacheza Bayern, ninapenda changamoto kwahiyo nachopitia ni jambo la kawaida, Ulikuwa msimu mgumu sana.”
Kane amefunga mabao 30 ya Ligi Kuu msimu uliopita. Ndiye mfungaji mwenye rekodi nzuri.