Ndugu na Jamaa wa viongozi wanao tenguliwa wametakiwa kuacha kulalamikia uamuzi wa mamlaka za uteuzi na badala yake wastahimili kinachofanyika.

Kauli hiyo ilitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo ametetea hatua yake ya kutengua viongozi mbalimbali wa Serikali mara kwa mara, akisema uamuzi huo unafanywa kwa lengo la kulinyoosha Taifa.

Rais Samia alisema hayo kutokana na mada iliyotolewa na Sheikh Sayyid Ayzuddin kutoka Kenya, aliyesema mafanikio ya Mtume Mohammad yalitokana na hatua yake ya kuwapa nafasi katika nyanja mbalimbali wale wanaostahili na si rafiki zake.

Akizungumza katika kongamano la wanawake wa Kiislamu kuelekea maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislamu 1445 Hijiria, alieleza kinachoangaliwa katika uteuzi na utenguzi ni kiongozi atakayefanya vizuri na asiyefanya, lakini kumekuwa na kelele nyingi wanapowaondoa wasiofanya vizuri.

“Tustahimili kuumia kwa mwanao kuondoka, mdogo wako kuondoshwa, tustahimili kuumia ili Taifa linyooke, vinginevyo tunyooshane tangu nyumbani, asifanye uzembe akaacha kazi akaenda vijiweni, sisi wakubwa huwa hatustahimili hayo, tuna mambo makubwa tumetoa ahadi ndani na kimataifa, tunataka wasaidizi wetu hawa watusaidie,” alisema.

Tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Tanzania Machi 19, 2021, Rais Samia ametengua viongozi mbalimbali na mara ya mwisho ni Julai 3, mwaka huu alipomtengua aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mwanahamisi Athumani na Wilaya ya Kilindi, Abel Busalama.

Juma Luizio kuibukua JKT Tanzania
Waarabu wampa jeuri Kocha Newcastle United