• Boniface Gideon – Tanga.

Mbunge wa Jimbo la Tanga (CCM), Ummy Mwalimu amesema fursa ya uchumi wa buluu itawanufaisha Wananchi wa Jiji la Tanga kwani wataweza kujipatia fursa ya shughuli mbalimbali ikiwemo kujiongezea kipato kwa ufugaji na kilimo kupitia bahari.

Ummy ambaye pia ni Waziri wa Afya, aliyasema hayo wakati alipotembelea miradi inayotekelezwa na Taasisi ya Tanga Yetu kupitia ufadhili wa Shirika la Botnar Foundation huku akiwashukuru kwa kukubali ombi lake kutekelezwa miradi hiyo, ambayo itasaidia kukuza uchumi wa buluu.

Alisema, kutokana na umuhimu wa uchumi wa buluu katika kukuza uchumi wa wananachi Jiji hilo limejipanga kuwa kinara katika uzalishaji wa majongoo bahari, unenepeshaji wa kaa pamoja na kilimo cha mwani kwa kutumia fursa ya bahari iliyopo kwenye Ukanda wa Pwani.

Waziri wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu (mwenye kilemba) akipokea maelezo kutoka kwa Mkandarasi Jitesh Jethwa, ambaye anayetekereza Ujenzi wa Bustani za mapumziko Jijini Tanga, maarufu Forodhani.

“Kwa sababu mkoa wa Tanga una eneo kubwa la bahari na tayari mafanikio yamekwisha kuyaona hivyo tumejipanga kuongeza uzalishaji Ili tuweze kuwa vinara wa kutumia fursa za uchumi wa buluu Kwa maendeleo ya watu wetu sambamba na nchi kupata mapato yake,”alisema Waziri Ummy.

Aidha ameongeza kuwa, “mimi kama Mbunge wa Jimbo la Tanga nitashirikiana na wadau Botnar Foundation kuendeleza kilimo cha mwani kikubwa tuwape elimu na ujuzi wananchi hususani wanawake ikiwemo kuwapa vitendea kazi ambayo vitasaidiaa kufanya vizuri katika kilimo cha Mwani na kutafuta masoko.”

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mwakilishi wa Botnar Tanzania, Dkt. Hassan Mshinda amemuhakikishia Mbunge Ummy kuwa wataendelea kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga katika kutatua kero za maendeleo hususan vijana na watoto.

Miradi hiyo ni ya uvuvi, kilimo cha mwani, jongoo bahari na unenepeshaji wa kaa pamoja na ufugaji wa samaki, kuku na kilimo cha mbogamboga katika kata za Tongoni, masiwani, Tangasisi, Usagara na Central, ambapo sehemu ya shilingi bilioni 5.65 zilizotumika zimewasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.

Viongozi 10 waliozibeba nchi zao Afrika – 8. Nnamdi Azikiwe
EWURA kuwachukulia hatua wanaoficha mafuta