Licha ya timu yake kupoteza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Esperance de Tunis ya Tunisia, Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssoupha Dabo, amesema anafurahi timu yake kupata nafasi ya kujipima na timu ‘ngumu’.
Azam FC iko imeweka kambi yake Tunisia kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Matajiri hao wa Chamazi, Dar es salaam pia watachuana kuwania Ngao ya Jamii na Kombe Shirikisho ‘ASFC’.
Dabo amesema kuwa anaendelea kukijenga kikosi chake na sasa wanajipanga na mchezo mwingine wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya US Monastir utakaochezwa leo.
Amesema kupitia mechi hizo, atapata nafasi ya kuangalia uwezo wa kila mchezaji wake na kupata kikosi chake cha kwanza.
“Nimehitaji kucheza mechi ngumu ili nifahamu kikosi changu kinatakiwa kujengwa zaidi katika nafasi gani, mechi hizo zitasaidia wachezaji wangu kuimarika na kupata uzoefu wa kutosha,” Dabo amesema.
Naye Afisa Habari wa Azam FC, Hashim lbwe, amesema timu yao inaendelea vizuri na maandalizi kuelekea msimu mpya wa 2023/2024 na anaamini watarejea nchini wakiwa na makali zaidi.
Ibwe amesema kocha wao ametaka kucheza mechi dhidi ya wapinzani wenye uwezo zaidi ili kuwapa wachezaji wake uzoefu kuelekea msimu mpya wa mashindano.
“Tukimalizana na US Monastir, mechi nyingine tumebaki nazo ni dhidi ya Etoile du Sahel, CS Sfaxien, zote za Tunisia, tunaamini tukirejea nyumbani, tutakuwa hatushikiki,” amesema lbwe.
Ikirejea nchini, Azam FC itakutana na Young Africans katika mchezo wa hatua ya Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii utakaochezwa Agosti 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini, Tanga.