Hakika katika Ulimwengu kuna mengi ya kujifunza, nakumbuka Babu yangu aliwahi kuniambia “Wajinga ni watu muhimu Duniani” maana kupitia wajinga hapo huwa tunawafahamu werevu, Babu alienda mbali zaidi akasema “Tabia ya mtu hujulikana akiwa nacho,” awali sikumuelewa lakini sasa naelewa.

Hapa Duniani tutaona na kujifunza vitu vingi vya kushangaza ambavyo wakati mwingine vinaweza kukufurahisha au kukuhuzunisha, nasema hivi kwa kukupa mfano wa Kijana mmoja wa zamani ambaye aliwahi kuwa rais wa nchi ya Sierra Leone kati ya Aprili 29, 1992 hadi Januari 16 , 1996 akiwa ndiye amiri jeshi mkuu na kiongozi wa ngazi ya juu kwenye taifa hilo lililopo kaskazini-magharibi mwa bara la Afrika.

Anafahamika kwa jina la Valentine Strasser, na aliingia madarakani akiweka rekodi ya kuwa kiongozi mwenye umri mdogo kuwahi kutokea, na hata sasa hakuna taifa ambalo limewahi kupata Mkuu wa Nchi mwenye umri chini ya miaka 25, ili avunje rekodi ya Strasser.

Ilikuwa ni Aprili 29, 1992 Strasser akiwa kijana Mwanajeshi mwenye umri wa miaka 25, aliwaongoza wanajeshi wenzake kuvamia Ikulu ya Sierra Leone, wakamteka aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Joseph Saidu Momoh, wakamlazimisha kukimbia naye akatorokea Conakry, nchini Guinea.

Baada ya Momoh kutorokea Conakry, Strasser alijitangaza kuwa Rais wa Sierra Leone na hapo maisha yake yakabadilika, akawa Mkuu wa Nchi, na kwa hali hiyo hakutaka kuishi kwenye nyoyo za Wasierra Leone tena, kwani kilichofuata hakulipa malimbikizo ya mishahara ya wanajeshi na watumishi wengine wa umma.

Akafuja almasi ya Sierra Leone, kwa vile jina lake ni Valentine, basi sikukuu ya Valentine’s Day akaifanya kuwa sherehe ya kitaifa yenye mapumziko, huyu ndiye Strasser kijana aliyekuwa na mbwembwe nyingi, alitamba sana bila kujua dira yake.

Mwaka 1993 katika mkutano wa Wakuu wa Serikali katika nchi za Jumuiya ya Madola, uliofanyika Limassol, Cyprus, alitinga kwa mbwembwe akiwa amevaa suruali ya jeans na fulana yenye maandishi Sunny Days in Cyprus (Siku za Jua Kali Cyprus).

Alikuwa mtu wa starehe, vurugu nyingi kwa wanawake, aliua watu wasio na hatia na Rais huyu Strasser alisahau kuwa ipo siku uongozi hautakuwa kwenye mikono yake na ambacho kinaweza kumfaa ni kuishi ndani ya mioyo ya watu, ili wamtetee na kumpigania baadaye.

Waswahili wanasema “Mbio za Sakafuni huishia ukingoni” hatimaye Januari 16,1996 Strasser alipinduliwa na msaidizi wake, Brigedia Jenerali Julius Maada Bio na Strasser akakimbilia Uingereza, huko akajiunga na Chuo Kikuu cha Warwick, kilichopo mjini Coventry, akaanza masomo ya sheria, akasema anataka awe wakili ili awatetee Waafrika.

Lakini mwaka mmoja wa masomo, Strasser aliishiwa fedha kilichofuata akaacha chuo na hapo maisha ya Uingereza yakawa magumu, akakimbilia Gambia nako kukawa pagumu, mwisho akarudi Sierra Leone, mjini Grafton, Mashariki ya Mji Mkuu wa nchi hiyo, Freetown.

Kazi ya kwanza ambayo Strasser aliifanya ikawa kuanzisha kichuo kidogo cha kufundisha kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), hilo nalo la maisha ya chuo likamshinda na hapo ndipo akakumbuka kuwa ana Mama yake.

Baada ya kila kitu kwenda kombo, Strasser alirudi nyumbani kwa mama yake mzazi na kuishi kwenye banda la uani na akiwa na umri wa miaka 49, akasahau ya Ikulu sasa akaanza kunywa pombe za kienyeji mtaani.

Hana hadhi yoyote kama kiongozi mkuu wa nchi mstaafu, Strasser anaishi kama mtu tu mtaani, Mlevi na hakuna anayemjali wala hana mtu wa kumtetea wala kumpigania kwa sababu hakuishi kwenye nyoyo za watu. Strasser ndiye Mkuu wa Nchi wa zamani, anayeishi kimaskini kuliko wote duniani.

Ukiwa kiongozi na kugeuka kituko kama Strasser inawezekana kabisa maana ukiishi vibaya na watu wasikupende, akija mtawala ambaye hatakutambua kama mkuu uliyepita, unaweza kuishi maisha ya hovyo kama ombaomba mtaani au mnywa gongo uliyeshindikana.

Sio Vibaya ukijifunza sasa kwamba ukiishi vizuri kama kiongozi, hata baada ya kutoka au kutolewa, jamii itakuenzi, itakupenda, kukupigania na kukutetea ukiwa nje ya ulingo na hutaishi vibaya. Ukiishi vibaya, utakuwa na mwisho mbaya kama Strasser.

Mwaka 2019, Kapteni Valentine Strasser aliruhusiwa Kutoka Hospitali nchini Ghana, hii ilikuwa ni siku moja mapema kuliko ilivyopangwa kwa sababu ya maendeleo yake ya kuimarika kiafya maana alipata nafuu baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu wake wa kushoto.

Alisafirishwa nje ya nchi akiwa hawezi kutembea lakini mpaka anaruhusiwa alitembea kwa msaada na akawa chini ya uangalizi katika kituo cha makazi na maajenti wa huduma ya siri wa Ghana wakimlinda lakini hata hivyo alikatwa mguu wake wa kushoto.

Katika mahojiano na Waziri wa Habari na Mawasiliano wa wakati huo nchini Sierra Leone, Mohamed Rahman Swarray, alieleza kuwa madaktari wanaomtibu Kapteni Strasser waliamua akatwe mguu wake baada ya kubaini kuwa alikuwa na ugonjwa wa kidonda katika eneo la mguu uliojeruhiwa.

“Zimwi likujualo halikuli likakwisha” ndivyo tunavyoweza kusema kwani mwamba huyu akapata walau kupewa huduma kwa heshima, akajengewa nyumba na kupewa stahiki zote kama kiongozi mstaafu, baada ya awali kuzongwa na aibu kubwa kumfika akiomba chakula mtaani na kuzurula hovyo akinyooshewa vidole.

Hata hivyo, Wakati sehemu ndogo ya wananchi wa Sierra Leone wakimkosoa Rais Bio kwa kumtuma Kapteni Mstaafu Strasser nchini Ghana na kumtunza kwa pesa za serikali, wakishikilia kuwa yeye ni mmoja wa viongozi wanaohusika na hali mbaya ya nchi hiyo.

Lakini asilimia kubwa ya Wananchi wanasema kama Mkuu wa zamani wa Nchi, Rais Bio ana jukumu la kumtendea hivyo kwa heshima Kapteni Strasser na kumsaidia kutoka katika hali mbaya kwa sababu alipigania amani, utu na ustawi wa Sierra Leone.

Yusuf Kagoma: Simba SC wajipange sana
Smith Rowe kumbadili Gabriel Jesus